Mwanadada Flaviana na harakati za kutatua kero ya elimu nchini, asaidiwa na PSPF
JINA la Flaviana Matata sio jina geni masikioni mwa watu hapa nchini hususan kwa wadau wa masuala ya ubunifu wa mavazi na mitindo kwa ujumla.
Flaviana alianza jitihada za kujitangaza katika medani ya mitindo mwanzoni mwa miaka ya 2000 hasa pale alipoukwaa ulimbwende wa Miss Universe.
Flaviana ni mwanadada mrefu, mwembamba, mcheshi na mzuri kwa ujumla wake anaonekana kuwa ni mwenye malengo katika fani yake ya uanamitindo hasa pale anapounganisha mitindo na kusaidia masuala ya elimu.
Anaamini kuwa uanamitindo sio lazima tu kuonekana jukwaani au katika vyombo vya habari na katika matangazo ya biashara peke yake.
Akizungumza na gazeti hili Flaviana anasema kuwa kwake uanamitindo ni kuchukua mwonekano mzuri anaokuwa akionekana kwenye majukwaa ya mitindo na kisha kuweka katika hali halisi.
Akiifafanua zaidi hoja hiyo anasema kuwa akiwa kama mwanamitindo ambae anawakilisha vema nchi nje ya mipaka, anaona kwa inatakiwa kujichukulia kama kioo katika jamii na kuanza jitihada za kuhamaisha mabadiliko kwenye jami.
Akiwa anaamini kuwa elimu nduo chanzo cha mabadiliko katika jamii anaichukulia umuhimu mkubwa elimu hiyo kwa kuanza kusaidia wanafunzi wenye uhitaji maalum.
Anaongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa sekta ya elimu kwa wanafunzi ameamua kuanzisha mradi wa utoaji wa vifaa vya elimu kwa wanafunzi hasa wale waliopo katika mazingira magumu.
Anasema kuwa mazingira hayo magumu kwa wanafunzi yanatofautiana kwa kuwa wapo ambao wanakosa faraja ya moyo huku wengine wakiwa wanakosa hata vifaa vya kujisomea wakiwa darasani.
Anaongeza kuwa chini ya mradi huo wanafunzi wanapatiwa madaftari, kalamu, mkebe, mabegi na misaada mingineo muhimu ya kimasomo.
"Mimi nimechagua elimu kama ndio njia mojawapo ya kuleta chachu ya mabadiliko katika jamii, na kwa kutambua hilo ninawasaidia wanafunzi walio katika elimu ya msingi na hadi sasa ni mengi nimeshayaanza kuyafanya"alisema Flaviana.
Katika kuonesha dhamira yake ya dhati katika kusaidia watoto wenye uhitaji huo maalum wa misaada ya shule mwanamitindi Flaviana anasema kuwa tayari kwa msimuu huu wa Januari ambapo wanafunzi wanarejea darasani amewasaidia wanafunzi 1000 vifaa hivyo vya shule.
Anasema kuwa misaada hiyo imetolewa kwenye shule ya msingi Chanzige iliyopo wilayani Kisarawe ambapo wamesaidiwa wanafunzi 280 pia wanafunzi 420 wa shule ya msingi Kimanzichana iliyopo Mkuranga.
Anaongeza kuwa wanafunzi wengine ni wa shule ya msingi Msinune iliyopo Bagamoyo ambapo wanafunzi 300 wamesaidiwa.
"Sasa unaweza kuona ni kwa jinsi gani ambavyo kuna wanafunzi wamesaidiwa kupitia mradi huu ambapo wanapewa vifaa hivyo kwa bure kabisa kila mmoja na tuanzidi kujipanga kuhakikisha kuwa mwezi Julai tunasaidia wengine wengi zaidi"anasema Flaviana.
Pia mwanadada huyu anasomesha wasichana 15 ambao wanapata elimu ya sekondari katika shule mbalimbali za serikali hapa nchini.
Katika kufanikisha adhma yake hiyo Flaviana amekuwa akisaidiwa na watu mbalimbali, mfano mzuri ni Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma(PSPF) pamoja na mdau wa masuala mitindo wa nchini Marekani Russell Simons.
Flaviana anaonekana kuwa na moyo wa kushirikiana na wadau wengine katika kufanya kazi hiyo ya kusaidia watoto wenye uhitaji maalum.
Akishirikiana na Russell Simons amepewa madaftari ya mazoezi na kalamu za wino kwa wanafunzi 500 walio chini ya mradi wa Tanzania Mitindo House, The Olevolos Project ya Arusha pamoja na shule ya msingi Mwasele mkoani Shinyanga.
Kwa msaada huo wa Russell Simons katika kila mwanafunzi kwenye wanafunzi hao 500 kila mmoja atapatiwa madaftari 10 na kalamu ya wino moja.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa PSPF, Hawa Kikeke anasema kuwa mfuko huo unatambu ajitihada zinazofanywa na wasanii katika kuleta mabadiliko kwenye jamii.
Anasema kuwa kazi ya uanamitindo aifanyao Flaviana ni moja kati ya walengwa wa mfuko huo ambao uanatambua pia wafanyakazi wasiokuwa kwenye mfumo rasmi wa ajira.
Anaongeza kuwa kwa kutambua jitihada zake za kuleta mabadiliko katika jamii PSPF imeamua kumuunga mkono katika kufanikisha msaada wake wa wanafunzi wa awamu ya kwanza ya mwezi Januari wa kutoa misaada kwa wanafunzi 1000.
"PSPF inatambua nafasi za wafanyakazi kama hawa katika suala zima la kusukuma mabadiliko kwenye jamii na ndio maana na sisi tumeona kuwa ni wakati pia wa kuungana nae"Anasema Hawa.
"Wasanii, wanamitindo na hata wajasiriliamali wadogowadogo hawa wanahitajika katika mfuko huu wa PSPF sasa ni kwa nini na sisi tusimuunge mkono mwanadada kama huyu ambae ni mwanamitindo na anasaidia jamii"anasema Hawa.
Flaviana anawataka watu mbalimbali kujitokeza na kumuunga mkono katika harakati hizo ambazo amesema kuwa ni kwa faida ya watanzani kwa ujumla.
zaidi msomeni Flaviana katika www.habari5.blogspot.com